Tetemeko la ardhi Uturuki: Mbwa aliyeokoa makumi ya watu katika tetemeko la Mwaka 2017 Mexico apelekwa Uturuki

Mexico inatuma baadhi ya mbwa wake maarufu wa utafutaji na uokoaji nchini Uturuki kusaidia kutafuta watu waliofukiwa chini ya vifusi kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu.

Ndege iliyokuwa na mbwa 16 ilipaa kutoka mji wa Mexico City mapema Jumanne.

Mexico, ambayo inakabiliwa na matetemeko ya ardhi, ina timu maalum za kiraia na kijeshi ambazo mara nyingi hutumwa kusaidia wakati majanga yanapotokea.

Mbwa hao walivutia mioyo ya watu wa Mexico wakati wa tetemeko la ardhi la 2017 nchini humo, walipookoa maisha ya watu kadhaa.

Mbwa anayeitwa Frida alipata umaarufu kimataifa alipoonekana akiwatafuta manusura katika Jiji la Mexico akiwa amevalia miwani na buti za kujikinga.

Jeshi la wanamaji lilimsifu Frida kwa kuokoa maisha ya watu 12 na kupata miili 40 katika operesheni katika nchi za Mexico, Haiti, Guatemala na Ecuador.

Wakati Frida alikufa kutokana na uzee mwaka jana, angalau mmoja wa mbwa wenzake waliokuweko katika tetemeko la Mexico la mwaka 2017 atakuwa sehemu ya timu ya Navy ya Mexico inayosafiri kwenda Uturuki.

Ecko, mbwa mwenye asili ya Ubelgiji, Malinois, alionekana kwenye uwanja wa ndege wa Mexico City akiwa na mhudumu wake wa jeshi la wanamaji.

Lakini mbwa hao hawapelekwi kijeshi tu. Kikundi cha utafutaji na uokoaji cha kiraia kinachoitwa Los Topos de Tlatelolco (The Moles of Tlatelolco) pia kiko njiani.

Kikundi cha wafanyakazi hao wa kujitolea wenye uzoefu mkubwa walikuwa wamemtumia ujumbe Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico Marcelo Ebrard kutaka kushiriki kutoa msaada wao.

Ndani ya saa chache, Bw Ebrard alijibu kwamba usafiri ulikuwa umepangwa kwa ajili yao kwa usaidizi wa ubalozi wa Uturuki katika Jiji la Mexico.

Mexico sio nchi pekee inayotuma mbwa kusaidia katika juhudi za uokoaji nchini Uturuki na Syria. Croatia, Jamhuri ya Czech, Ujerumani, Ugiriki, Libya, Poland, Uswizi, Uingereza na Marekani pia zinapeleka mbwa na wakiwa na waongozaji wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *